Dylan Kerr aachana na Gor Mahia
Zikiwa zimebaki wiki 3 msimu mpya wa ligi kuu nchini Kenya kuanza kutimua vumbi, kocha wa mabingwa watetezi Gor Mahia Dylan Kerr ametangaza kujiuluzu nafasi yake katika timu hiyo.
Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier ameiambia tovuti ya timu hiyo kuwa, wamepokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa Kerr na wamekubali maamuzi yake na kumtakia kila la kheri katika kazi yake mpya.
Katika barua hiyo Kerr ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Gor Mahia amewashukuru viongozi,wachezaji na mashabiki wa timu hiyo na kueleza kuwa anajiunga na timu nyingine katika msimu huu mpya.
Kocha huyo wa zamani wa Simba SC ya Tanzania, alijiunga na Gor Mahia Julai 2017. Akaiongoza timu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo, 2017 na 2018
Hili ni pigo kwa Gor Mahia kumpoteza Muingereza huyo wakiwa wanajiandaa na msimu mpya wa ligi na pia michuano ya klabu bingwa Afrika ambapo katika hatua ya awali wanacheza na Nyassa Big Bulles Novemba 27