Marko Arnautovic aitaka Klabu Bingwa Ulaya
Mshambuliaji Marko Arnautovic ameweka wazi kuwa yupo tayari kuondoka West Ham ili kufukuzia ndoto yake ya kucheza michuano ya klabu bingwa Ulaya.
Akizungumza na gazeti la nchini kwao Austria ‘ Kurier ‘ akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, Arnautovic alisema : “ Nina miaka 29, huo ni umri mzuri. Ni wazi ninataka kushindana wachezaji bora. Lakini katika jambo hili ninamuamini kabisa kaka yangu “
Kaka yake Danijel ambaye ndiye wakala wake, hajakataa uwezekano wa mchezaji huyo kuihama timu hiyo ya London Mashariki.
“ Tayari anacheza ligi kuu ya England na hapo ndio wachezaji bora wapo. Lakini kwa mchezaji kama Marko hii si mwisho . “ alisema Danijel
“ Marko yupo tayari kwa hatua ijayo. Mchezaji kama yeye hatakiwi kucheza ili kutoshuka daraja. Anatakiwa kucheza michuano ya kimataifa.
Alipoulizwa kuhusu Marko anaweza kuondoka mwezi Januari akajibu : “ Hilo linawezekana. Lilikuwa karibu sana, sana majira ya kiangazi yaliyopita “
Arnautovic amejiunga na West Ham kutoka Stoke City kwa pauni milioni 25 mwaka 2017 na amekuwa ni kipenzi cha timu hiyo , akifunga magoli 11 katika ligi kuu msimu jana na msimu huu akiwa amefunga matano.
Imeripotiwa kuwa West Ham imezuia uhamisho wowote wa mchezaji huo kwa mwezi Januari.