Kamati ya uchaguzi haitambui kurudi kwa Manji Yanga, Uchaguzi kama kawaida Januari 13 2019.
Uongozi wa Klabu ya Yanga Afrika leo umetangaza kuitisha mkutano Mkuu wa dharura wa klabu hiyo tarehe 24 Novemba, ajenda bado ikiwa haijawekwa wazi ila inadaiwa kuwa ni kuweka azimio la pamoja la uchaguzi mkuu wa klabu hiyo usiguse nafasi ya mwenyekiti.
Yanga kwa sasa wapo katika mvutano na kamati ya uchaguzi ya shirikisho la mpira Tanzania (TFF) ambao inawataka Yanga kufanya uchaguzi mkuu kuwachagua viongozi wa nafasi mbalimbali lakini wao hawakubaliani na hilo kwa madai kuwa mwenyekiti wao Yusuf Manji bado yupo katika nafasi hiyo.
Baada ya mwenyekiti wa baraza la wadhamini Yanga George Mkuchika jana kutangaza kuwa amepokea barua ya Yusuf Manji kutaka kuendelea na nafasi yake hiyo kama kawaida, barua ikionesha kuandikwa toka mwezi Agosti 1, leo mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa TFF Malangwe Mchungahela kupitia radio Uhai FM amethibitisha kuwa mchakato wa uchaguzi mkuu Yanga upo pale pale January 13 2019 hakuna kilichobadilika, Manji kama angetaka kurudi angesema mapema na angetoka barua.
“Utaratibu tumetangaza anayetaka kugombea aende TFF akachukue fomu, uchaguzi unaendelea vile vile na nafasi ya mwenyekiti ipo wazi na uchaguzi umepangwa Januari 13 2019 ndio utafanyika, siku zote alikuwa wapi hadi uchaguzi umetangazwa ndio anaandika barua?”alisema Mchungahela.