CORONA KUKATA MSHAHARA WA MESSI NA WENZAKE
Kwa mujibu wa ripoti za nchini Hispania, baadhi ya nyota wa klabu ya Barcelona wapo tayari kukatwa mishahara yao katika kipindi hiki cha virusi vya Corona ambapo ligi imesimama.
Ripoti hizo zinasema Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu amefanya mazungumzo na Lionel Messi,Sergio Busquets,Jordi Alba na Sergi Roberto kuhusu kupunguzwa mishahara yao na kikao hicho inaaminiwa kufanikiwa na makato hayo yanaweza kutokea.
Kutokana ugonjwa huu wa mlipuko, klabu hazijapoteza mapato kwenye viingilio na pesa za haki za matangazo ya televisheni tu, bali na mapato yatokanayo na udhamini,uuzaji wa vifaa vya michezo, utalii katika makumbusho na mapato kutoka kwenye matukio mengine ambayo yanafanywa katika viwanja.
Pia imeelezwa kuwa mazungumzo hayo ya uongozi wa klabu na nyota hao yapo vizuri licha ya kuwa makubaliano ya mwisho hayatakamilika mpaka iwe wazi kuwa ni lini msimu wa 2019/20 utarejea na kwa masharti gani.