Ushirikiano wa Neymar na Cavani, unamuongeze msongo wa mawazo Henry
Hakuna lugha rahisi inayoweza kutumika kwa sasa kuelezea hali ya timu ya AS Monaco inayoendelea katika maisha yake ya mashindano tofauti tofauti, ikiwa ni timu ambayo imeanza kuzoea kukubali vipigo visivyomalizika mfululizo.
Monaco msimu huu inaondolewa kama ni timu yenye ushindani na kuanza kuitwa kibonde baada ya leo tena, kukubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya PSG, licha ya kuaminiwa kuwa sapoti ya mashabiki katika uwanja wao wa nyumbani Louis II inaweza kusaidia kuinusuru timu hiyo na vikipigo ndani ya Ligue One.
Ushirikiano mzuri wa Neymar aliyefunga bao moja dakika 64 kwa mkwaju wa penati, ushirikiano wake na Edinson Cavani umeimaliza Monaco kwani Cavani alifunga hat-trick akifunga mabao kuanzia dakika ya 4 alipopewa pasi na Neymar na dakika ya 11 na 53 akakamilisha hat-trick na kuiteketeza AS Monaco chini ya kocha wao Thierry Henry.
PSG bado anaendelea kutawala Ligue One kwa kuongoza Ligi hiyo kwa alama 39, akishinda michezo yote 13 wakati Monaco inaendelea kudidimia mkiani ikiwa na alama saba nafasi ya 19 sawa na Guingap aliyepo nafasi ya 20 kwa kuwa na alama saba sawa na Monaco, Thierry Henry sasa anashindwa kuipa ushindi Monaco katika Ligue One katika mchezo wowote katika michezo yake minne ya mwanzo kwa mara ya kwanza toka Didier Deschamps akutane na changamoto hiyo mwaka 2001, Henry katika michezo minne ya Ligue One kama kocha wa Monaco amepoteza michezo mitatu na kutoka sare mchezo mmoja.