SHABIKI WA CHRISTIANO RONALDO, MDUKUZI AMBAYE AMEWAPELEKEA KIFUNGONI MAN CITY
Rui Pinto ndio jina ambalo klabu ya Manchester City wanalichukia zaidi kwa sasa. Kwa nini? , kwa sababu huyu ndiye mbaya wao.
Rui Pinto ni mdukuzi (hacker) ambaye alidukua mfumo wa emails za klabu mbalimbali barani Ulaya na kupeleka habari kutoka kwenye email hizo kuzichapisha katika jarida la Ujerumani Der Spiegel
Baada ya kuchapishwa ndipo UEFA wakatumia taarifa hizo kuichunguza Manchester City kuhusu kuvunja sheria ya ‘Financial Fair Play’ na kupelekea kuwafungia kushiriki michuano ya Ulaya kwa muda wa miaka miwili.
Pinto,31, sasa yupo jela tangu Machi mwaka jana na anataraji kupandishwa kizimbani huko kwao nchini Ureno kujibu mashitaka zaidi 90 yanayohusiana na udukuzi, hujuma na unyang’anyi.
Pinto ambaye amejizolea umaarufu mkubwa na kupendwa na watu, ndiye aliyevumbua hati za mwanamke tajiri zaidi Afrika Isabel Do Santos,ambazo zinaonesha jinsi mwanamke huyo alivyopata utajiri wake kwa unyonyaji na ufisadi kwa nchi yake Angola.
Isabel,46, ni mtoto wa kwanza wa Rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos Santos.
Licha ya kufichua hati hizo, Pinto hakudai hela yoyote za malipo na wanasheria wake wamekuwa wakisisitiza kuwa Pinto ni mtu ambaye ni wa muhimu sana kwenye kupaza sauti za kusema ukweli.
Pinto ambaye wanamuita “The Computer Genius” —alizaliwa katika kitongoji cha Porto Vila Nova de Gaia huko Ureno, alijifunza mwenyewe Kompyuta,na hakuwahi kupata elimu ya juu kuhusu kompyuta.
Alipokuwa ana umri wa miaka 23,alidaiwa kuidukua benki iliyopo Cayman Islands na kuiba dola 330,000.
Hata hivyo Pinto alikataa kufanya hivyo, lakini akakiri kudukua data ambazo zilikuwa zinaonesha “Jinsi visiwa vya Cayman vilivyotumika kwa ukubwa katika kukwepa kodi na kutakatisha fedha.”
Akiwa nchini Hungary akiishi huko na kumsaidia biashara ya vitu vya kale baba yake, Pinto alikamatwa na polisi wa Hungary mwezi Januari mwaka jana kwa kumtuhumu kudukua mfumo wa kampuni ya uwekezaji katika michezo inayoitwa Doyen Sports.
Waendesha Mashitaka wa Ureno walisema Pinto alikuwa anailaghai kampuni hiyo akiwataka wampe kati ya Euro 500,000 na Milioni moja, ili asichapishe taarifa zao ambazo amezidukua
Baadae Pinto akajibu kuwa ni kweli alikuwa anawasiliana na kampuni hiyo ya uwekezaji lakini ni “kwa ajili tu ya kuhakikisha kuwa wakiri wamefanya makosa na pia kujua ni shilingi ngapi walikuwa tayari kulipa kwa ajili ya taarifa hizo zisichapishwe”
Pinto ambaye ni shabiki wa FC Porto na Cristiano Ronaldo alisema kuwa alitaka kuwafichua wahusika wakuu wa maovu katika soka.
Mara baada ya kukamatwa kwake, wanasheria wake walisema kuwa Pinto ana mapenzi na soka na amekuwa akikereka sana na vitu ambavyo amekuwa anaendelea kuvitambua.
Pinto amekuwa akilaumu mamlaka za Ureno kwa kuendelea kujaribu kumnyamazisha na kumzuia kushirikiana na nchi za Ulaya.
Pinto amekuwa akiungwa na mkono na watu wengi ambao wamekuwa wakishinikiza aachiwe huru kufuatia vitendo vyake vya kuvumbua maovu kwa manufaa ya watu wote bila ya kutaka malipo.
Hata mashabiki wa Borussia Dortmund wamewahi kuonesha bango (Banner) likioneshwa kupinga kukamatwa kwa Pinto.
Pinto akizungumza na jarida la Ujerumani Der Spiegel mwezi uliopita alikiri kujua hatari ya kazi yake ya kupaza sauti kusema ukweli, akisema kuwa amekuwa hata akipokea vitisho vya kuuliwa kupitia mtandao wa Facebook.
“Nilikuwa ninatambua kila kitu kinaweza kutokea. Nilijua mamlaka za Ureno hushitaki wapaza sauti za ukweli. Kwa hiyo nikawa tayari. Mamlaka za Ureno wanaogopa kwa kile ninachojua.”—— Alisema Pinto ambaye anasubiri kusomewa mashitaka ambayo yanaweza kumpelekea hukumu ya miaka 10 jela.