Barcelona hali tete Nou Camp, imevunja rekodi ya miaka 20
FC Barcelona kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20, wameruhusu rekodi yao ivunjwe katika ardhi ya Catalunya uwanja wao wa Nou Camp wakiwa wenyeji wa Real Betis katika mchezo wa 12 wa Ligi Kuu Hispania (LaLiga) 2018/2019.
Jiji la Barcelona lilipozwa na Real Betis siku ya Jumapili ya Novemba 11 baada ya kuifunga timu hiyo nyumbani kwao kwa idadi ya mabao 4-3, mabao ya Real Betis yakiwekwa wavuni na Junior, Joaqui, Lo Celso na Sergio Canales dakika ya 83.
Jitihada za kuchomoa za Barcelona hazikuzaa matunda na hatimae wakaishia kufunga mabao matatu tu yaliofungwa na Lionel Messi aliyefunga mabao mawili dakika ya 68 kwa mkwaju wa penati na dakika za nyongeza baada ya Arturo Vidal kufunga bao la pili dakika ya 79.
Kichapo cha mabao 4-3 nyumbani hakijawaondoa Barcelona kileleni mwa msimamo wa LaLiga, wamebaki na alama zao 24 wakati Real Betis wakipanda hadi nafasi ya 12 wakiwa na alama 16 ila Barcelona baada ya kufungwa leo wanakuwa wametofautiana alama nne na wapinzani wao Real Madrid ambao hawakuanza vizuri Ligi hiyo wakiwa na alama 20 wakikaa nafasi ya 6.
Barcelona kichapo cha leo kinawafanya wavunje rekodi yao ya kutokufungwa na Real Betis kwa miaka 20, kabla ya mchezo wa leo Barcelona walikuwa hawajawahi kufungwa na Betis katika uwanja wa Nou Camp toka mwaka 1998, toka mwaka huo Barcelona wamecheza na Real Betis katika uwanja huo mara 17 wakishinda mara 15.