ARSENAL YAILAZIMISHA SARE CHELSEA NYUMBANI
Chelsea wakiwa nyumbani dhidi ya Arsenal, hii ilikuwa ni mechi ya 200 kwa timu hizi kukitana katika mashindano yote. Chelsea waliingia katika mchezo huu wakiwa hawajapoteza mchezo wowote wa nyumbani katika mechi 7 zilizopita huku Arsenal wakiingia na rekodi ya kutokuwa na ushindi katika mechi 7 zilizopita za ligi katika uwanja wa Stanford Bridge (D1, L6) mechi ya mwisho wakishinda Oktoba 2011 kwa goli 5 – 3 katika mchezo ambao makocha wote wa sasa Mikel Arteta na Frank Lampard walicheza mechi hiyo kipindi wakiwa wachezaji.

Chelsea ndiyo iliyoanza kupata goli la kuongoza likifungwa na Jorginho kupitia mkwaju wa penati iliyosababishwa na David Luiz aliyemchezea madhambi Tammy Abraham na kupelekea beki huyo wa Arsenal kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Akiipatia Arsenal goli la kusawazisha dakika ya 63, Gabrieli Martinelli amekuwa kinda wa kwanza chini ya miaka 20 kufunga goli 10 ndani ya msimu mmoja tokea afanye hivyo Nicolas Anelka msimu wa mwaka 1998/99.
Chelsea walirudi na kuongoza kwa goli la Ceaser Azpilicueta dakika ya 84 kabla ya Hector Bellerin kuisawazishia Arsenal dakika ya 87 na mechi hiyo kuisha kwa sare ya goli 2 – 2.