Mwenyekiti wa uchaguzi TFF kaongea kwa wanaopanga kuharibu mchakato Yanga
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Malangwe Ally Mchungahela leo amefanya mkutano na waandishi wa habari na kuzungumzia suala zima la mchakato wa uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga Afrika.
Malangwe Ally ameeleza mbele ya waandishi wa habari kuwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa Yanga licha ya kukumbwa na changamoto tofauti tofauti lakini mchakato upo pale pale kama kawaida walivyotangaza awali.
Kwa sasa kumekuwa na mvutano kwa baadhi ya wanachama wa Yanga hawataki kufanya uchaguzi wakidai kuwa bado wanaimani na kuamini kuwa Yussuf Manji licha ya kutangaza kujiuzulu wanatambua kama mwenyekiti wao hadi sasa.
“Mchakato wa uchaguzi wa Yanga ulishaanza tayari tangu tulipoutangaza tarehe tano na fomu zilikuwa zianze kuchukuliwa tarehe nane lakini tarehe nane hatukuweza kwa sababu tulikuwa na kikao na wajumbe wa kamati ya uchaguzi wa Yanga na tukakubaliana baadhi ya masuala fomu zikatoka tarehe 9 wakati mchakato wa uchaguzi huu ukiendelea tuna taarifa baadhi ya viongozi wa kamati ya utendaji ya Yanga wanataka kuharibu mchakato wa uchaguzi”