GSW WASHINDA MECHI YA KWANZA KWENYE UWANJA WAO MPYA
Baada ya misimu 48, Golden State Warriors wamehama uwanja wa Oracle Arena uliopo Oakland, California na sasa wanatumia uwanja mpya Chase Center uliopo San Fransisco, California.
Tangu wahamie katika uwanja wao mpya, ambao wameanza kuutumia rasmi katika msimu huu wa NBA, walikuwa hawajawahi kushinda mechi hata moja kati ya nne walizokuwa wamecheza nyumbani.
Si Steph Curry au Draymond Green ambaye ameleta ushindi huo wa kwanza nyumbani, ni mchezaji mpya katika ligi ya NBA (Rookie) Eric Paschall.
Leo katika mechi hiyo ambayo Warriors wameibuka na ushindi wa Pointi 127-118 dhidi ya Portland Blazers ya Damian Lillard, Eric Paschall ambaye alikuwa akisheherekea siku yake ya kuzaliwa akitimiza umri wa miaka 23, aliibuka nyota wa mchezo akifunga Pointi 34, Rebounds 13, na Pointi tatu 4.

Huu ni ushindi wa kwanza wa Golden State Warriors katika uwanja wao mpya Chase Center.
“Ile ilikuwa ni uchizi kidogo. Siwezi kudanganya” alisema Paschall kuhusu mashabiki wa Warriors kumuimbia kuwa ni ‘MVP’.
“Kiuwazi,kwa mchezaji mpya katika ligi, unasikia unaimbiwa MVP…..ile ilikuwa wakati mzuri . Nilikuwa nimeweka mkazo kwenye mechi kwa sababu nilikuwa kama hivi, ‘ Sawa sawa tuna nafasi ya kushinda sasa hivi,’ lakini kusikia (Kuimbiwa hivyo) , acha niwashukuru Dub Nation, kiukweli, kwa kuniamini mimi.”
Warriors inakabiliwa na wimbi la majeruhi wa mastaa wao, Steph Curry ambaye amefanyiwa upasuaji wa mkono wake wa kushoto hivi karibuni, Klay Thompson ambaye atarejea mwezi Februari anauguza mguu wake , Draymond Green ameumia kidole na D’Angelo Russell ameumia kifundo cha mguu
Mpaka sasa Warriors wamecheza jumla ya mechi saba katika NBA msimu huu, wakishinda mechi mbili na kupoteza mechi tano.