UNAI AMVUA XHAKA UNAHODHA ARSENAL
Baada ya mgogoro wa Graint Xhaka na mashabiki katika mechi ya sare ya 2 – 2 dhidi ya Crystal Palace, kocha Unai Emery ametangaza kumvua unahodha mchezaji huyo.
“Nilikuwa na kikao nae na nikamueleza hatokuwa tena Nahodha, alikubali na alielewa.
Nilihitaji kufanya maamuzi na sasa hilo limeisha.” Alisema kocha Unai Emery.
Nafasi hiyo ya Unahodha sasa imechukuliwa na mshambuliaji Pierre Emerick Aubameyang aliyevaa kitambaa hicho katika mchezo wa mwisho wa Arsenal wakilazimishwa sare dhidi ya Wolves.

Xhaka alionyeshwa kukerwa na kitendo cha kuzomewa na mashabiki pale alipokuwa akifanyiwa mabadiliko katika mechi dhidi ya Crystal Palace na kufikia hatua ya kuivua jezi na kuitupa kisha kwenda moja kwa moja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Kocha Unai Emery baadae alisema mchezaji huyo anajua amekosea na anatakiwa kuomba mashabiki msamaha jambo ambalo mchezaji huyo hakuafiki moja kwa moja , lakini baada ya siku chache aliandika ujumbe akielezea tukio hilo kupitia mtandao wa Instagram na kuomba msamaha.
Xhaka alielezea juu mya kejeli na vitisho anavyopata toka kwa mashabiki wengi ikiwa kupitia mitandao ya kijamii na vingine kuelekea kwa familia yake, na hivyo ndivyo vilimpelekea kufanya vitendo hivyo kwa mashabiki kwa hasira.