BIFU LAKE NA GREEN LILICHANGIA DURANT KUONDOKA WARRIORS
Nyota wa NBA Kevin Durant amethibitsha uhusiano wake mbaya na mchezaji mwenzake Draymond Green ulichangia aondoke Golden State Warriors.
Durant na Green wote wakiwa Warriors, mwezi Novemba mwaka jana walirushiana maneno baada ya Draymond Green kupata Rebound katika mechi dhidi ya LA Clippers na kukataa kumpa pasi Durant ambaye alikuwa wazi mechi ikiwa 106-106 sekunde chache kabla ya kuisha, baadae Warriors walipoteza mechi hiyo.
Tukio hilo lilipelekea wachezaji hao kugombana katika vyumba vya kubadilishia nguo,na baadae Warriors kumfungia mechi moja Green.

Baada ya kupoteza fainali za NBA dhidi ya Toronto Raptors, Durant aliondoka Warriors na kujiunga na Brooklyn Nets licha ya kuwa hatacheza msimu huu wote kutokana na kuwa majeruhi.
Katika mahojiano na ESPN Durant jana aliulizwa kuhusu kama uhusiano wake na Green kama ulichangia kuondoka Warriors alijibu “ Ndio, kidogo. Ndio kwa hakika.

“ Kama mchezaji mwenzako anaongea na wewe vile, unafikiria kuhusu hilo kidogo. Nilihisi kama nahitaji kubadilika na vitu vingi vya Golden State vinaenda ukingoni na nikahisi vitu vinaenda mwisho. “