USM ALGER HALI TETE KIUCHUMI, INAWEZA KUTANGAZWA KUFILISIKA
Klabu ya USM Alger ya nchini Algeria ipo katika kipindi kigumu na inatarajiwa kuna uwezekano mkubwa kutangazwa kuwa imefilisika kwa miezi ya baadae kufuatia kuyumba kiuchumi kwa muda sasa.
Hali hiyo imefikia kufuatia mfanyabiashara na mmiliki wa timu hiyo Ali Haddad kufungwa Jela toka Machi 2019 kwa kukutwa na makosa kadhaa nchini humo.

Ali Haddad yupo jela kutokana na kudaiwa kutenda makosa ya kumiliki hati mbili za Algeria za kusafiria (Passport) kitu ambacho ni kinyume na sheria, kukutwa na kiasi kikubwa cha pesa taslimu za kigeni kitu ambacho ni kinyume na sheria.
Makosa mengine ni uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, Ali Haddad pamoja na wafanyabiashara wengine waliokuwa karibu na Rais wa zamani wa Algeria Abdelaziz Bouteflika mali zao zimezuiliwa.

Ni wazi sasa klabu haiwezi kulipa mishahara ya wachezaji na wafanyakazi wengine kitu kilichopelekea mwezi Oktoba wachezaji kugoma ila mgomo ukamalizwa baada ya matatizo ya kifedha kutatuliwa na moja kati ya mashabiki wa timu hiyo (tajiri) kuchangia pesa.
Matatizo ya kiuchumi na kifedha yalioikuta klabu hiyo, yalipelekea pia kidogo klabu hiyo ishindwe kusafiri kwenda Kenya kucheza mchezo wao wa kuwania kufuzu kucheza Klabu Bingwa Afrika.