Kama Kroenke asipomuuzia Dangote Arsenal, Dangote haoni hasara kubadili mawazo
Moja kati ya ndoto kubwa ya tajiri namba moja Afrika Alhaji Aliko Dangote ni kutaka kuinunua klabu ya mpira wa miguu ya Arsenal yenye makazi yake jijini London Uingereza, Dangote raia wa Nigeria ni moja kati ya mashabiki wakubwa wa Arsenal wanaotokea bara la Afrika.
Dangote baada ya kuomba kuinunua klabu hiyo kwa zaidi ya mara moja kwa nyakati tofauti, bado anaamini kuwa ana nafasi ya kuimiliki timu hiyo anayoishabikia lakini kwa sasa anasema kama watashindwa kumuuzia atatafuta klabu nyingine ya kununua hawezi kuendekea kusubiri.
Kwa sasa Arsenal inamilikiwa na Stan Kroenke ambaye amekuwa akishawishiwa mara kwa mara na Dangote aiuze klabu hiyo kwa bilionea huyo namba moja wa Afrika, kama Kroenke ataendekea kukataa Dangote atanunua klabu nyingine ya soka.
Awali Dangote alitangaza kuwa atarudi na ofa nono ambayo anaamini Arsenal hawatoikataa baada ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda chake kikubwa Lagos Nigeria cha kusafishia mafuta, mradi ambao ulikuwa unamuhitaji awekeze pesa nyingi, hivyo sasa yupo vizuri kiuchumi zaidi ya ilivyokuwa mwanzo, kama hufahamu tu Kroenke sasa anamiliki karibia hisa zote za Arsenal baada ya kununua asilimia 30 ya hisa za bilionea wa kirusi Alisher Umanovic mwezi Agosti kwa dau linalotahwa kufikia pound bilioni 1.8