HAKUNA MAREFU YASIO NA NCHA,UBABE WA WARRIORS UMEFIKA UKINGONI
Waswahili wanasema hakuna marefu yasio na ncha, huku wazungu wakiwa na msemo wao wakisema “All good things must come to an end”, wakimaanisha kuwa vitu vyote vizuri lazima viishe.
Baada ya kutawala ligi ya NBA kwa muda mrefu, wakienda fainali za ligi hiyo tangu mwaka 2015 mpaka mwaka huu 2019, Golden State Warriors sasa wanaonekana fungate yao ya muda mrefu inaelekea ukingoni.

Leo wakiwa katika uwanja wao mpya Chase Center, wamepokea kichapo cha Pointi 110-121 kutoka kwa Phoenix Suns, na kufanya mpaka sasa wawe wamepoteza mechi tatu na kushinda moja tu katika msimu huu wa NBA.
Kikosi chao baada ya kuondokewa na moja nyota wao mkubwa Kevin Durant aliyeenda Brooklyn Nets, kilianza msimu kikiwa dhaifu, wakimkosa nyota wao mwingine Klay Thompson ambaye ameumia mguu na kutarajiwa kurejea mwezi Februari mwakani.

Sasa kidonda chao kimezidi kuingiwa na mchanga huku mikono yao ikiwa imefungwa nyuma na kamba za katani, leo katika mechi dhidi ya Phoenix Suns, zikiwa zimebaki dakika nane robo ya tatu kumalizika, Steph Curry akiwa anaelekea kufunga, aligongana na Aron Baynes wa Suns na kuanguka chini na kuumia mkono wake wa kushoto.
Curry mara moja akaenda katika vyumba vya kubadilishia nguo, na timu yake kuthibitisha kuwa MVP huyo mara mara mbili wa NBA amevunjika mkono wake wa kushoto.

Steph Curry anataraji kufanyiwa kufanyiwa vipimo zaidi leo Alhamisi kutambua ni kwa muda gani atakuwa nje akijiuguza.
Kwa hali ambayo walikuwa nayo Warriors wakiwa na Steph Curry msimu huu, ni dhahiri kuwa wanaenda kuwa moja ya timu mbovu katika ukanda wa Mashariki kipindi hiki ambacho watamkosa nyota huyo.