VAR IMEIKATILI DHAMIRA YA WATANZANIA DHIDI YA LIVERPOOL
Mbwana Samatta sasa anastahili kupata heshima zote katika soka Tanzania, haya ni mawazo ya baadhi ya watanzania kupitia mitandao ya kijamii wakati Samatta akiwa nahodha wa KRC Genk katika mchezo wa kihistoria dhidi ya Liverpool.
Mchezo huo unakuwa wa kihistoria kwa Tanzania kutokana na kudaiwa kuwa ndio mchezo wa kwanza wa Samatta kuwahi kufuatiliwa zaidi akicheza ngazi ya klabu kutokana na wengi kuwa na kiu ya kutaka kujua Samatta atafunga goli kwenye ukuta wa beki bora wa Ulaya Virgil van Dijk.
Samatta atafanya nini dhidi ya wachezaji wanaowania tuzo ya Ballon d’Or lakini furaha ya watanzania kumuona Samatta akifunga ilikatishwa na VAR (video assistant referee) baada ya dakika ya 26 kufunga goli kwa kichwa lililopelekea mchezo kusimama dakika kadhaa.
Goli hilo lilikataliwa baada ya VAR kounesha mtoaji wa pasi ya mwisho Junya Ito alikuwa ameotea wakati anapokea mpira kabla ya kuupiga kwa Samatta ambaye kutumia kichwa chake aliuweka kwenye nyavu za kipa bora wa Ulaya Allison Becker.
Mechi hiyo iliisha kwa Liverpool kushinda kwa goli 4-1 ,mabao ya Chamberlain aliyefunga mawili, Sadio Mane na Mohamed Salah ndio yalizamisha jahazi la Genk ambao walipata bahati ya kufunga la kufutia machozi dakika ya 88 kupitia kwa Odey.
Genk wanashika mkia katika kundi E kwa kuwa na alama 1, Napoli akiongoza kwa alama 7 akifuatiwa na Liverpool wenye alama 6 wakati RB Salzburg akiwa nafasi ya tatu kwa alama 3.