MESSI ANAANDIKA REKODI MPYA LIGI YA MABINGWA ULAYA
Usiku wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Oktoba 23 ulikuwa ni usiku wa kihistoria kwa nahodha wa FC Barcelona Lionel Messi ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kilichocheza dhidi ya Slavia Praha.
Mchezo huo ambao Barcelona walikuwa ugenini walishinda kwa magoli 2-1 Lionel Messi akifunga la kwanza dakika ya 3, la pili dakika 57 Peter Olayinka akajifunga ikiwa ni dakika 7 zimepita toka Boril afunge goli la kusawazisha.
Barcelona ilifanikiwa kuondoka na alama 3, Lionel Messi yeye akaondoka na rekodi mpya katika mchezo huo kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga goli katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu 15 mfululizo toka alipocheza kwa mara ya kwanza 2004 dhidi ya Shakhtar Donetsk.
Messi pia anaingia katika rekodi ya kuvifunga jumla ya vilabu 33 kwenye michuano hiyo, sawa na Cristiano Ronaldo na Raul Gonzalez.
Ushindi huo unaiweka Barcelona kileleni mwa Kundi F kwa kuwa na alama 7 ikifuatiwa na Dortmund wenye pointi 4, na Inter wakishika watatu nao wakiwa na pointi 4.