MCHEZAJI ATIMULIWA NICE BAADA YA KUIBA SAA
Klabu ya Nice ya nchini Ufaransa imemfukuza mshambuliaji wake Lamine Diaby-Fadiga,18, baada ya kukiri kuiba saa ya mchezaji mwenzake Kasper Dolberg yenye thamani ya Dola 76,000 (Tsh Milioni 174).
Lamine amethibitisha aliiba saa hiyo aina ya Rolex katika vyumba vya kubadilishia nguo Septemba 16, na akisema kitendo hicho alikifanya kutokana na wivu.
Baada ya Mfaransa huyo kukiri kuiba, Nice walitangaza kuvunja nae mkataba na sasa amesajiliwa na klabu ya daraja la pili Paris FC.
Dolberg,21, amejiunga na Nice katika majira ya kiangazi mwaka huu akitokea Ajax, wakati Lamine alikuwa Nice tangu akiwa na umri wa miaka 14.
Baada ya kutimuliwa,Lamine kupitia ukurasa wake wa Twitter alieleza wivu ulivyosababisha kufanya kitendo hicho kwa mchezaji mwenzake ambaye wote wanacheza nafasi ya ushambuliaji.
Lamine alieleza kuwa kukaa majeruhi kwa miezi kadhaa na wivu kutokana na mafanikio ya Dolberg tangu atue klabuni hapo ndivyo vilimsukuma kufanya hivyo.
“Ninajivunia kuvaa jezi ya timu yangu ya utotoni msimu uliopita katika Ligue 1.
Kwa bahati mbaya niliumia kwa miezi kadhaa na kurudi kwangu katika ushindani kulicheleweshwa zaidi kufuatia kadi nyekundu niliyoipata nilipocheza mechi ya chini ya miaka 19”.
Hivyo viliniathiri kiakili na hali yangu ngumu ikawa tofauti kabisa na mafanikio ya Kasper (Dolberg), mchezaji mwenzangu.
Nikaichukua na kuelekeza kwake bila ya sababu yoyote ya kufanya hivyo, labda kwa sababu ya wivu.”
“Badala ya kujaribu kupambana uwanjani kumpa ushindani ili kupata nafasi, nikamfanyia upumbavu” aliandika Lamine Diaby na pia akaomba msamaha kwa mashabiki na watu wote waliokuwa wanampenda.