HAMILTON ASHINDA RUSSIAN GP, UKAIDI WAMPONZA SEBASTIAN VETTEL
Lewis Hamilton amefanikiwa kushinda mbio za Russian Grand Prix baada ya mgogoro baina ya madereva Sebastian Vettel, Charles Leclerc na uongozi wa timu ya Ferrari.
Hamilton amefuatiwa na dereva mwenza Veltteri Bottas katika nafasi ya pili, Charles Leclerc aliyeanza katika nafasi ya kwanza ‘pole position’ akimaliza katika nafasi ya tatu.
Nafasi ya nne imechukuliwa na Max Verstapen wa RedBull aliyeanza katika nafasi ya tisa baada ya kupigwa penati kutokana na gari lake kufanyiwa maboresho mengi mapya ya ufundi.
Mgogoro wa Ferrari ulianza mapema baada ya Charles Leclerc aliyeanza katika nafasi ya kwanza kutekeleza maelekezo toka kwa uongozi wa timu wa kumwachia dereva mwenza Sebastian Vettel ampite mapema. Hii ni mbinu iliyokuwa imelenga kuhakikisha madereva wote wa Ferrari wanakuwa katika nafasi mbili za juu kuepusha Lewis Hamilton kuchukua nafasi yeyote kati ya hizo.
Mambo yalibadilika baada ya Sebastian Vettel kukaidi kumwachia Leclerc arudi katika nafasi yake. Hata baada ya kupatiwa maelekezo kwa njia ya radio mara kadhaa dereva huyo aligoma kwa kuwaambia wasimamizi wa timu yake wamwambie Leclerc aongeze spidi kwani hata yeye anaweza kushinda. Hili liiwalazimu timu ya Ferrari kubadilisha mikakati kuanzia kwa Leclerc kubadili matairi kabla ya muda waliopanga.
Hii haikusaidia kwani Vettel alipata matatizo ya kiufundi na kupelekea kushindwa kumaliza mbio yote haya yakiwapa nafasi madereva wa Mercedes kumaliza katika nafasi mbili za juu kwa mara ya kwanza tokea wafanye hivi British Grand Prix katikati mwa mwezi Julai.