LEEDS NA MARCELO BIESLA WALIVYOSHINDA TUZO YA FIFA FAIR PLAY
Leeds United na kocha wao Marcelo Biesla wameshinda tuzo ya FIFA Fair Play 2019 kufuatia kitendo cha uungwana walichokionesha katika mechi yao dhidi ya Aston Villa msimu uliopita.
Mchezaji wa Aston Villa Jonathan Kodjia akiwa amelala chini baada ya kuumia, Leeds waliendelea na mchezo na Mateusz Klich kufunga goli liliowafanya wenyeji Leeds kuongoza kwa goli 1-0.
Licha ya mechi hiyo kuwa muhimu, Leeds wakihitaji ushindi ili waweze kupata nafasi ya kupanda daraja kuingia katika ligi kuu kwa mara ya kwanza tangu washuke mwaka 2004, kocha wao Marcelo Biesla aliwaambia wachezaji wake wawaachie wapinzani wao wakafunge katika hali ya kuonesha uungwana katika michezo.
Aston Villa wakaanzisha mpira na kwenda kufunga goli la kusawazisha kupitia Albert Adomah.
Mechi iliisha kwa sare ya 1-1 na Leeds kuwapa Sheffield United nafasi nzuri ya kupanda daraja moja kwa moja na wao kwenda kwenye Playoffs ambapo wakashindwa kupanda daraja na kubaki kwenye Championship.