SABABU INAYOMFANYA JOSE MOURINHO AAMINI ETO’O ALISTAHILI BALLON d’Or
Kocha wa zamani wa vilabu vya Man United, Real Madrid, Chelsea na Inter Milan Jose Mourinho hadi leo haamini kwa nini mshambuliaji wa zamani wa Barcelona na Inter Milan Samuel Eto’o hakuwahi kushinda tuzo ya Ballon d’Or.
Mourinho ambaye alifanya kazi na Eto’o katika klabu ya Inter Milan wakishinda Treble msimu wa 2009/10, anaamini kwa uwezo aliokuwa nao Mcameroon huyo alistahili kubeba tuzo ya Ballon d’Or walau mara moja.
“Amecheza fainali tatu za Ligi ya Mabingwa mbili kati ya hizo amecheza na FC Barcelona na zote amefunga na ameshinda moja akiwa na Inter na kutwaa mataji mengi ya ligi, alikuwa mshambuliaji bora duniani kwa miaka kadhaa, ninafikiri alistahili Ballon d’Or, lakini hilo jambo lipo nje ya uwezo wetu” alisema Mourinho katika mahojiano na Redio ya Cameroon.

Eto’o ,38, ametangaza kustaafu kucheza soka hivi karibuni akiwa amecheza michezo 759 ngazi ya klabu katika mashindano yote na kufunga mabao 370, Barcelona pekee Eto’o alifunga mabao 130 katika michezo 199 ya mashindano yote na kushinda mataji 8, Inter akifunga mabao 52 katika michezo 103 akishinda mataji 6 na mataji mawili ya AFCON akiwa na timu yake ya Taifa Cameroon (2000 na 2002)