AVEVA NA KABURU DHAMANA IPO WAZI ILA WARUDISHWA RUMANDE
Leo imetangazwa taarifa kuhusiana na aliyekuwa Rais wa klabu ya Simba SC Evans Aveva na makamu wake Godfrey Nyange Kaburu kuwa baada ya kuwa rumande kwa muda mrefu sasa wanaweza kupata dhamana.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa nafasi ya dhamana kwa Kaburu na Aveva baada ya kuondolewa kwa mashtaka ya tuhuma za utakatishaji fedha ambapo kwa kawaida kosa hilo halina dhamana.
Mahakama imeamuru kuwa dhamana sasa ipo wazi kwa Kaburu na Aveva ila kwa sharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Tsh milioni 30, washtakiwa hao sasa wanashtakiwa kwa makosa 8 baada ya utakatishaji fedha kufutwa.
Kaburu na Aveva kesi yao ambayo ipo chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wamerudishwa rumande hadi kesho Septemba 20 watakapoanza kujitetea.
Kaburu na Aveva wamerudi rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana wakisema kuwa hawakujiandaa hivyo kuanzia kesho wanaweza kupewa wakitimiza masharti hayo.