TANZANIA YAFUZU HATUA YA MAKUNDI SAFARI YA QATAR 2022
Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania imefanikiwa kuingia katika hatua ya makundi ya kufuzu michuano ya kombe la Dunia 2022 Qatar baada ya kuitoa Burundi kwenye raundi ya awali.
Tanzania imeshinda mchezo huo kwa Penati 3-0 baada ya sare ya 1-1 katika dakika 120 ndani ya dimba la uwanja wa Taifa.
Tanzania ndio ilikuwa ya kwanza kupata goli kupitia kwa Nahodha wake Mbwana Samatta katika dakika ya 29 kabla ya Abdul Feiston kuisawazishia Burundi katika dakika mbili za nyongeza za kipindi cha kwanza
Mechi hiyo ilienda mpaka dakika 120 kufuatia mechi ya kwanza iliyopigwa Burundi Jumatano hii Septemba 4 kuisha kwa sare ya 1-1.
Juma Kaseja leo kwa mara nyingine ameibuka shujaa wa penati akiokoa penati ya kwanza ya Burundi huku zingine mbili wakizipiga nje ya goli.
Kaseja anafanya hivi ikiwa imepita mwezi mmoja tangu aiongoze Tanzania kuingia raundi ya pili ya kufuzu michunao ya CHAN 2020 kwa kuitoa Kenya kwa mikwaju ya penati 4-1 nchini kwao.
Sasa Tanzania inakuwa ni moja ya timu 40 za Afrika zilizo katika raundi ya pili ya kufuzu michuano hiyo kombe la Dunia 2022, timu hizo zitagawanywa katika makundi kumi, kila kundi likiwa na timu nne.