NADAL AWAFUATA FEDERER NA DJOKOVIC RAUNDI YA 4 US OPEN
Baada ya kujiondoa katika mashindano ya Cincinnati Masters mwezi uliopita kutokana na uchovu, mjadala kuhusu uzima wa Mhispania huyu juu ya majeraha sasa hauna nafasi baada ya kuonyesha kiwango chake cha hali ya juu katika mechi zake mbili US Open.
Nadal amefanikiwa kwenda hatua ya raundi ya 4 baada ya kumshinda Mkorea Kusini Chung Hyeon kwa seti 6-3, 6-4, 6-2.
Bingwa huyu wa grand slam mara 18 na mchezaji namba 2 kwa ubora duniani anaungana na bingwa mtetezi Novak Djokovic na bingwa wa grand slam mara 20 Roger Federer katika hatua ya raundi ya 4.
Mwaka uliopita Nadal alilazimika kuishia katika nusu fainali baada ya kushindwa kuendelea na mechi dhidi ya Juan Martin del Potro kutokana na jeraha la goti.
Katika mchezo wa raundi ya nne utakaopigwa kesho Septemba 2 Nadal atakutana na bingwa wa US Open mwaka 2014 Mcroatia Marin Cilic.