YANGA YAANDIKA HISTORIA BOTSWANA NA KUFUTA UTEJA
Timu ya Yanga SC imefanikiwa kuandika historia nchini Botswana baada ya kufanikiwa kulipa kisasi katika michezo ya klabu Bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers.
Yanga baada ya kutoka sare ya 1-1 nyumbani katika mchezo wa kwanza, walienda Gaborone kucheza mchezo wa marudiano na kupata ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa wavuni na Juma Balinya kunako dakika ya 43 ya mchezo na kudumu kwa dakika zote 90.
Kwa matokeo hayo Yanga wanafuzu raundi ya kwanza ambapo watacheza dhidi ya Zesco ya Zambia waliofika hatua hiyo baada ya ushindi wa jumla ya goli 3-0 dhidi ya Green Mamba ya Eswatini.
Ushindi huo wa Yanga ni sawa na kulipa kisasi baada ya Machi 17 2018 kuondolewa na Township Rollers katika michuano hiyo.
Mwaka 2018 Yanga waliondolewa na Township Rollers katika michuano hiyo hatua za kuwania kucheza makundi baada ya mchezo wa Dar es Salaam Yanga kufanya makosa na kupoteza 2-1 na alipokwenda Gaborone akatoka droo 0-0 na Township kukata tiketi ya kucheza hatua ya Makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia.