UONGOZI WA LIGI KUU NCHINI ENGLAND WAKATAA KUWAONGEZEA CITY MEDALI
Ombi la Man City kuongezewa medali za ubingwa wa ligi kuu msimu uliopita limekataliwa.
Man City walipewa jumla ya medali 40 baada ya kushinda kombe la ligi kuu msimu jana kwa ajili ya wachezaji wote waliocheza mechi zaidi ya tano, meneja wao pamoja na benchi la ufundi, lakini klabu hiyo ilituma maombi ya kuongezewa medali kwa ajili ya wachezaji wao vijana.
Uongozi wa ligi kuu umetupilia mbali maombi hayo na kudai kuwa medali walizopewa zinawatosha.
Kocha wa City Pep Guardiola mwezi Mei baada ya kubeba ubingwa, alisema kuwa kuna wachezaji vijana sita ambao walikuwa wakifanya mazoezi na kikosi tangu mwanzo mpaka mwisho wa msimu, licha ya kukosa nafasi ya kucheza kutokana na maamuzi yake, lakini anaona ni ajabu kutopewa medali kwa sababu nao ni mabingwa.
Pep Guardiola amewahi kupinga vikali sheria hiyo ya kucheza zaidi ya mechi tano ndio upewe medali.