WAKALA KATHIBITISHA DEMBELE AMEZIPIGA CHINI OFA KIBAO
Ousmane Dembele ,22, hana mpango wa kuihama FC Barcelona katika kipindi hiki cha usajili cha majira ya joto licha ya kuletewa ofa kutoka vilabu mbalimbali Ulaya, hii ni kwa mujibu wa wakala wake.
Dembele alijiunga na FC Barcelona 2017 akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya pauni milioni 97 akitazamiwa kama ndio mbadala sahihi wa Neymar aliyekuwa kaondoka wakati huo na kujiunga na PSG ya nchini Ufaransa.
“Ninataka kutolea ufafanuzi suala la Dembele, hana mpango wa kuondoka Barcelona kwa sasa, huu ni mjadala ambao ulishafungwa miezi kadhaa nyuma na hakuna viashiria vya kubadilika kwa hilo, Dembele anajisikia vizuri kuwa ndani ya klabu hii (Barcelona) licha ya kupokea ofa kutoka klabu kubwa mbalimbali Ulaya” alisema wakala wa Dembele Moussa Sissoko akihojiwa na gazeti la Ufaransa la L’Equipe
Dembele kwa sasa yupo nje ya uwanja kwa muda wa wiki tano kufuatia kusumbuliwa na misuli ya paja aliyoyapata ijumaa iliyopita katika mechi dhidi ya Athletic Bilbao.