KINDA ALIYEWAHI KUFANYA MAJARIBIO MAN UNITED KAJITOA UHAI WAKE KISA KUANDAMWA NA MAJERUHI
Kinda aliyewahi kufanya majaribio katika klabu ya Man United Joel Darlington amejiua kwa kujinyonga baada ya kuandamwa na majeraha ya muda mrefu katika maisha yake ya soka ambayo yalimpelekea kutokuwa sawa kiakili.
Imethibitishwa kuwa Machi 18 mwaka huu kaka wa mchezaji huyo Kyran alimkuta mdogo wake amejiua katika gereji ya nyumbani kwao Gellifor Kaskazini mwa Wales huku akiacha ujumbe wa sababu zake za kujiua.
Mshambuliaji huyo inaripotiwa kuwa alizidi kusumbuliwa na tatizo la wasiwasi baada ya kupata matatizo (majeraha) ya mgongo yaliompelekea pia kuachana na chuo ambapo alikuwa analenga kuja kuwa mwalimu wa utimamu wa mwili kwa wanasoka.
Kinda huyo ambaye aliwahi kuichezea Bala Town ya ligi Kuu ya Wales alikuwa anatazamiwa kuja kuwa nyota mkubwa wa soka kutokana na uwezo wake, hiyo inatokana na kuitwa katika timu ya vijana ya Wales, lakini pia kufanya majaribio katika klabu kubwa kama Manchester United lakini majaribio hayo yaliisha baada ya kupata jeraha la kuvunjika mkono.