ANDY RUIZ JR ‘CHIBONGE’ KAGOMA KUSAINI ANATAKA DAU LIONGEZWE AMRUDIE ANTHONY JOSHUA
Moja kati ya mapambano yanayotazamiwa kuwa na mvuto mkubwa ni pambano la marudiano kati ya bondia Mmexico Andy Ruiz Jr na Bondia Muingereza Anthony Joshua.
Bondia Andy Ruiz tayari alishakubali kulipwa Pauni Milioni 8 katika pambano hilo la marudiano, makubaliano yalifanya kabla ya hata pambano la kwanza kufanyika ambapo Mmexico huyo aliushangaza Ulimwengu kwa kumpiga AJ kwa TKO raundi ya saba.
Andy Ruiz ameripotiwa kukataa kusaini mkataba wa pambano hilo la marudiano akitaka pesa ya malipo izidi Pauni Milioni 8 (Tsh Bilion 22) ambayo awali walikubaliana.
Pambano hilo la marudiano linatarajiwa kupigwa Disemba 7 mwaka huu katika mji wa Diriyah Saudi Arabia.
Andy Ruiz anayeshikilia Ubingwa wa IBF, WBA na WBO lazima arudiane kupigana na Anthony Joshua kufuatia Muingereza huyo kutumia kipengele kilichopo katika mkataba wao uliopita kuomba pambano la marejeano.
Awali Joshua kabla ya kupigana na Andy Ruiz alikuwa apigane na bondia Jarrel Miller ambaye aliondolewa baada ya kufeli vipimo vya dawa zisizohitajika michezoni, waandaaji wa pambano la marudiano nchini Saudi Arabia wameweka Pauni Milioni 33 ( Tsh Bilioni 91) kwa ajili ya kuwa wenyeji pambano hilo.
Katika pambano la kwanza iliripotiwa kuwa AJ alilipwa Tsh Bilioni 49 huku mpinzani wake ambaye ndiye aliibuka mshindi akilipwa Tsh Bilioni 13.