Claude Leroy kamuita tena Adebayor
Kocha wa timu ya taifa ya Togo Claude LeRoy amemuita mshambuliaji Emmanuel Adebayor kwenye kikosi cha wachezaji 23, kitakachokua na jukumu la kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za AFCON 2019 dhidi ya Algeria.
Claude LeRoy amemjumuisha mshambuliaji huyo, licha ya kukataa kucheza katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali hizo mwezi Oktoba dhidi ya Gambia, kwa madai ya kutoridhishwa na mazingira ya uwanja wa nyasi bandia mjini Lome.
Akitangaza kikosi hicho kocha LeRoy alithibitisha kuwa yeye na Adebayor walishafanya mazungumzo na atacheza mchezo ujao katika uwanja huo alioukataa awali kwa kudai mazingira mabovu.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa pia amewaita kikosini wachezaji wanaocheza soka katika ligi ya Togo Ouro-Akoriko Sadate na Wilson Akakpo ili kuziba nafasi za Djene Dakonam na Ouro-Sama Hakim ambao wanatumikia adhabu ta kuonyeshwa kadi za njano.
Bila ya uwepo wa Adebayor katika kikosi cha Togo mwezi October, Togo iliambulia sare ya bao moja kwa moja nyumbani mjini Lome, na siku chache baadae waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gambia ugenini.
Matokeo hayo yaliiacha Togo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D kwa kuwa na alama 5, baada ya kucheza michezo minne, huku wakizidiwa alama mbili na vinara wa kundi hilo Algeria na Benin.
Timu ya taifa ya Togo (The Sparrow Hawks) itahitaji ushindi dhidi ya Algeria ili kufanikisha azma ya kuongoza msimamo wa kundi D, ambalo kwa sasa linaongozwa na Mbweha wa Jangwani (Algeria).
Kikosi cha Togo kilichotajwa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Algeria.