PSG kumpa adhabu Neymar Jr
Siku kadhaa baada ya uongozi wa klabu ya PSG kusema hawatakubaliana na utovu wa nidhamu toka kwa mchezaji wao yeyote, sasa klabu hiyo imeripotiwa kutaka kumpatia nyota wao Neymar adhabu ya kumkata bonasi ya mshahara wake baada ya kushindwa kuwasili katika mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.
Imeelezwa kuwa PSG wamelitilia mkazo suala hilo wakidai kuwa hakuna makubaliano yoyote kwa yeye kuendelea kukaa Brazil baada ya michuano ya Copa America kumalizika.
Kwa mujibu wa kituo cha Sky Sports, Neymar anapokea zaidi ya Pauni 500,000 ( Tsh Bilioni 1.4) kwa wiki na bonasi yake inawezekana kuzidi Pauni 100,000 ( Tsh Milioni 287). Msemaji wa Neymar mwanadada Day Crespo amesema mchezaji huyo atarejea klabuni hapo tarehe 15 ya mwezi huu baada ya tamasha la tarehe 13 lililoandaliwa na taasisi ya msaada mchezaji huyo nchini Brazil.
.
“ Taasisi ya Neymar imeandaa tamasha hili kwa miaka mitano sasa na kila mmoja anajua hizi tarehe. Baada ya tarehe hizo atarejea klabuni Julai 15, kama alivyoipa taarifa klabu wiki kadhaa nyuma” alisema mwanadada huyo Day Crespo.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa michezo wa PSG Leonardo ameweka wazi kuwa nyota huyo anaweza ondoka endapo tu klabu itapata ofa wanayohitaji huku akisema tayari kuna mazungumzo ya juu juu na klabu ya Barcelona.