Siasa zamzuia Shaqiri kucheza mechi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Winga Xherdan Shaqiri ameachwa katika kikosi cha Liverpool kitakachokwenda nchini Serbia kucheza mechi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Red Star Belgrade kesho jumanne.
Xhaqiri ameachwa katika kikosi hicho cha Jurgen Klopp kwa sababu za kisiasa na uhasama utakaoweza kutokea endapo atakwenda kucheza nchini humo.
Winga huyo wa Switzerland aliwakasirisha zaidi Waserbia katika kombe la Dunia mwaka 2018 baada ya kufunga goli dhidi yao na kushangilia kwa staili ya kuweka mikono kifuani ikiwa imepishana na kuweka alama “Double headed eagle” ambayo ipo kwenye bendera ya Albania.
Staili hiyo ya ushangiliaji inatokea kwenye bendera ya Albania nchi ambayo Serbia ina matatizo nayo ya kisiasa , hivyo Serbia wakapokea vibaya kitendo hicho.
Shaqiri alizaliwa Kosovo , yeye na familia yake walikimbilia Switzerland mwaka 1992 kama wakimbizi.
Kosovo ilidai uhuru wake mwaka 2008, na ina serikali yake inayotambulika na UN, lakini Serbia haitambui uhuru huo.
Serbia haitambui uhuru wa jimbo lake hilo la zamani Kosovo, ambalo idadi ya watu wake Milioni 1.8 ni kabila la Albania.
Shaqiri yeye alipoulizwa kwa nini alishangilia hivyo alisema hisia zilimfbya afanye hivyo na haihusiana na siasa, ni mpira tu .
Shaqiri alizomewa na mashabiki wa Red Star kila alipogusa mpira kwenye mchezo wa kwanza Anfield wiki mbili zilizopita. Hivyo katika kuzuia balaa zaidi, Liverpool wameamua mchezaji huyo asiende huko Serbia katika mchezo huo.
“ Tumesoma na kusikia fununu kuhusu namna ya mapokezi ya Shaqiri yatakavyokuwa na hatujui ni kipi kitatokea, tunataka kwenda huku tukiwa na mawazo asilimia 100 kwenye mpira na si kufikiria kuhusu kitu kingine “ amesema kocha Jurgen Klopp.
Liverpool inahitaji kushinda mchezo huo ili kujiweka vizuri zaidi katika kundi C ambalo yupo kileleni wakiwa na Pointi 6, Napoli wakiwa nafasi ya pili na pointi 5, nafasi ya tatu wakiwa PSG na pointi 4 huku Red Star wakiwa mkiani na pointi moja.