Kocha Herve Renard aachana na Morocco
Kocha Herve Renard amechana na timu ya Taifa ya Morocco zikiwa zimepita siku chache tangu timu hiyo kutolewa kwa mikwaju ya penati na Benin katika hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2019 inayoendelea huko Misri.
Mfaransa huyo alijiunga na Morocco Februari 2016 na mkataba wake ulitaraji kumalizika June 2022, lakini kocha huyo ameamua kufikia makubaliano na shirikisho la soka la nchi hiyo kuvunja mkataba baina yao.
Renard ameiongoza Morocco katika mechi 43, ambapo waliibuka na ushindi katika mechi 23, sare 9 na kupoteza 11.
Pia aliiwezesha Morocco kufuzu michuano ya kombe la Dunia mwaka 2018, ikiwa ni mara ya kwanza kufuzu michuano hiyo tangu mwaka 1998.
Herve Renard tayari ameshawahi kushinda kombe la AFCON mara mbili, akiwa na Zambia 2012 na Ivory Coast 2015.
Kocha huyo sasa anahusishwa kujiunga na timu ya Taifa ya Afrika Kusini pamoja na kurejea Ghana ambapo aliwahi kuwa mkufunzi wa viungo mwaka 2008.