Mayweather atangaza kurudi ulingoni mwaka huu.
Bondia wa Marekani Floyd Mayweather ametangaza rasmi kuwa atapigana na ‘ kickboxer’ Mjapan Tenshin Nasukawa katika mkesha wa mwaka mpya mjini Saitama, nchini Japan.
Mayweather,41, ambaye ameshinda mapambano yote 50 aliyowahi kupigana, ametangaza pambano hilo baada ya kusaini dili na kampuni ya Mixed Martial Arts ya Japan, RIZIN .
Mfumo na sheria zinazotumika katika pambano hilo bado hajizatajwa.
Nasukawa mwenye umri wa miaka 20, anashindana katika mapambano ya RIZN Fighting Federation, katika mapambano ya Kickboxing ameshinda yote 27 aliyopigana, huku kwenye MMA ameshinda pia ameshinda yote manne aliyopigana.
“ Ilikuwa ni ofa ya kushangaza lakini nilikubali bila ya kusita “ alisema Nasukawa
“ Ni wakati mkubwa katika maisha yangu na ninataka kuwa mtu anayebadilisha historia. Nitafanya hayo kwa hizi ngumi – angalieni tu “
Floyd Mayweather ambaye anaanza mazoezi ya pambano hilo kesho jumanne nchini Marekani ameeleza maamuzi ya kupigana pambano hilo nchini Japan.
“ Nilitaka kufanya kitu fulani tofauti. Ninataka kuonesha uwezo wangu nje ya US na kuwa kwenye pambano maalumu. “ amesema bondia huyo.
“ Nimepigana mapambano yangu yote 50 Marekani. Nikiwa kama Professional sikuwa na nafasi ya kutoka nje ya US kuonesha uwezo wangu na kuonesha kipaji changu duniani. “
“ Ninatazamia kuwapa burudani Disemba 31, lakini uhusiano wangu na RIZIN hautaishia hapo tu. Ninatarajia kuendelea sehemu mbalimbali za dunia “
Vile vile bondia huyo ambaye pambano lake mwisho alimpiga Conor McGregor Agosti 2017, amesema kuwa mfumo na sheria zitakazotumika kwenye pambano hilo zitatangazwa katika wiki chache zijazo.