Wachezaji wa Uganda walipwa baada ya mgomo
Wachezaji wa timu ya Taifa ya Uganda jana Julai 2 waligoma kufanya mazoezi huko nchini Misri ambapo wapo kwenye michuano ya AFCON wakishinikiza kulipwa bonasi na posho wanazodai shirikisho lao la soka FUFA.
Baada ya mgomo huo shirikisho hilo la soka jana limethibitisha kuwalipa wachezaji hao madai yao.
Kila mchezaji amelipwa Dola 14,600 kwa posho za ushindi pamoja na bonasi.
Kwa ushindi wao dhidi ya DR Congo kila mchezaji amelipwa Dola 4000 na kila Dola 2000 kwa sare dhidi ya Zimbabwe.
Kila mchezaji amelipwa Dola 420 kwa kambi ya siku 14, Dola 5,100 kwa kambi ya siku 34 Abu Dhabi na zaidi ya hapo, kila mchezaji amelipwa Dola 2,780 ikiwa ni ya kuongeza hamasa ya kambi na pia Dola 300 kwa mechi yao ya kirafiki dhidi ya Ivory Coast.
Hivyo Jumla kila mchezaji mpaka jana alipokea kiasi cha USD 14,600 sawa na Tsh Milioni 33.5.
Katika hatua ya 16 bora Uganda watacheza na Senegal Ijumaa hii Julai 5, na endapo watashinda kila mchezaji atapata Dola 5,000.
Na wakishinda robo fainali kila mchezaji atapata 7,000 , ushindi wa nusu fainali Dola 9,000 na wakishinda fainali ni Dola 14,630.