Patrick Aussems kaleza siri ya ushindi wa Simba kila mechi
Simba SC baada ya ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya klabu ya JKT Tanzania katika uwanja wa Mkwakwani Tanga, kocha wao mkuu Patrick Aussems aliongea na waandishi wa habari na kuelezea kuhusiana na mabadiliko ya timu yake ambayo amekuwa akishafanya katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu.
“Kama utakuwa umefuatilia michezo yote ya Simba kwa wiki nne au tano zilizopita nimekuwa nikifanya mabadiliko ya wachezaji na kila siku nimekuwa nikifanya kitu kile kile kwa sababu nawaamini wachezaji wangu, ukiachilia mbali uwanja, mpinzani wetu na ninachokiona mazoezi naweza kubadilisha kikosi, leo nimebadilisha wachezaji wapya watatu na tumeendelea kushinda hivyo ni kitu kizuri” alisema Patrick Aussems.
Patrick Aussems pia alilalamikia uwanja kabla ya kuanza kwa mchezo siku kadhaa nyuma kupitia mtandao wake wa twitter na kueleza kuwa eneo la kuchezea sio zuri ukizingatia ndio mara yake ya kwanza kukanyaga uwanja huo toka aanze kuifundisha Simba.
Ushindi wa magoli 2-0 ya Meddie Kagere dakika ya 13 na 38 yanaipa Simba alama tatu na kuwafanya wafikishe jumla ya alama 26 wapo nafasi ya pili nyuma ya Azam FC waliopo nafasi ya kwanza kwa alama 27 na wamecheza michezo sawa 11.