Esperance watetea ubingwa kimagumashi
Esperance ya Tunisia imetetea ubingwa wao wa Klabu Bingwa Afrika baada ya timu ya Wydad Casablanca kutoka Morocco kukataa kuendelea na mchezo kufuatia goli lao kukataliwa na mwamuzi ambaye alikataa kwenda kuangalia kwenye VAR ili kuthibitisha.
Mechi iliyochezwa jana nchini Tunisia, wakati Esperance wanaongoza kwa Aggregate ya 2-1, Wydad wakafunga goli la kusawazisha dakika ya 59 kupitia Ismail El Haddad, hata hivyo mwamuzi Bakary Gassama akakataa goli hilo akisema kuwa kulikuwa na makosa katika utengenezaji wa goli hilo na pia akaamua kutoangalia VAR kuthibitisha maamuzi yake.
Hii ilileta mzozo na kupelekea wachezaji wa Wydad kugoma kuendelea kucheza, wachezaji wabenchi na benchi la ufundi wakaingia uwanjani kumzonga mwamuzi huku mashabiki wa Esperance wakaanza kurusha vitu kwenye benchi la Wydad.
Baadae mzozo ulivyotulia bado wachezaji wa Wydad wakagoma kuendelea na mchezo wakiendelea kubishana na mwamuzi huyo kutoka Gambia.
Baadae Rais wa shirikisho la soka Afrika Ahmad Ahmad akatelemka mpaka uwanjani na kuongea na mabosi wa timu zote mbili,lakini hakuna kilichosuluhishwa na dakika 30 zikawa zimepita tangu mtafaruku huo kuanza. Rais huyo baadae akaenda kuongea na mwamuzi wa mchezo.
Gassama baadae akawapa onyo Wydad waendelee na mechi lakini wakaendelea kukataa, wachezaji wakawa wamekaa kwenye benchi na wengine wakiwa wanacheza mpira upande mwingine wa uwanja.
Baada ya saa moja na dakika 25 kupita tangu mzozo huo kuanza, Gassama akapuliza filimbi kuashiria mechi imetelekezwa na Esperance wakatangazwa kuwa mabingwa.