Hata kama hatocheza Lesotho, Amunike ataenda nae tu Samatta
Siku chache zijazo Taifa Stars itakuwa inajiandaa kuelekea Afrika Kusini kuweka kambi ya siku kadhaa kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza michuano ya mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon.
Taifa Stars itakuwa kambini nchini Afrika Kusini kwa sababu ya kutaka kuzoea hali ya hewa ya Afrika Kusini ambayo kwa kiasi kikubwa inashabihiana na hali ya hewa ya nchi ya Lesotho ambapo itacheza mechi Novemba 18 2018 mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu.
Ni wazi Taifa Stars itacheza mchezo huo bila uwepo wa Nahodha wao Mbwana Samatta ambaye anatumikia adhabu ya kuoneshwa kadi mbili za njano alizozipata wakati wa michezo dhidi ya Cape Verde, Azam TV imefanya mahojiano na kocha mkuu wa Taifa Stars Emmanuel Amunike na kutaka kufahamu atamuita Samatta licha ya kuwa hatocheza kwa ajili ya kuipa hamasa timu?
Amunike ameeleza kuwa Samatta hata kama hawezi kucheza mchezo dhidi ya Lesotho lakini atajumuika na timu kwa ajili ya kuleta hamasa ya mchezo huo ”Tutajumuika nae kama klabu yake itampa ruhusa maana huo utakuwa uamuzi wa klabu” kocha Amunike alisema katika mahojiano na Azam TV.
Taifa Stars ipo Kundi L ambalo linaundwa na timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde na inahitaji ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Lesotho ili kujiweka nafasi nzuri ya kufuzu michuano ya Afrika 2019, Tanzania ipo nafasi ya pili katika Kundi L ikiwa na alama tano ikiongozwa na Uganda wenye alama 10. Na kama Tanzania itaifunga Lesotho na Uganda ataifunga Cape Verde basi Tanzania itakuwa na nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 38 toka iliposhiriki mara ya mwisho 1980 Lagos Nigeria.