Wenger na Mourinho wakutanishwa meza moja
Wakati vita ya kuwania Ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya itakuwa ikiendelea katika Dimba la Wanda Metropolitano Jumamosi hii,Juni Mosi, kuna vita nyingine itakuwa inafanyika nje ya uwanja.
Ni vita ya mafahari wawili, Jose Mourinho na Arsene Wenger ambao kwa mara ya kwanza watakuwa pamoja wakichambua mechi katika studio za beIN SPORTS.
Makocha hao ambao wote wamekuwa wakifanya uchambuzi katika kituo hicho msimu huu lakini kwa nyakati tofauti, Jumamosi hii watachambua mechi hiyo ya fainali itakayozikutanisha timu zote za England, Liverpool na Tottenham.
Makocha hao wamekuwa na uadui wakati wakiwa wanafundisha katika ligi ya England, na hivyo baada ya kituo hicho kutoa taarifa hiyo, imewafanya wadau wa soka kuwa na shauku kubwa kuwaona wakiwa meza moja kwa mara ya kwanza.