Mwamuzi afungiwa na CAF miezi 6 kwa kuboronga fainali
Shirikisho la mchezo wa mpira wa miguu barani Afrika (CAF) limeendelea kuhakikisha marefa na waamuzi wa mchezo wa soka wa kiafrika wanakuwa makini kwa CAF kuwa wakali na kuwaadhibu yanapotokea mapungufu.
.
Kufuatia mchezo wa kwanza wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Wydad Casablanca ya nchini Morocco dhidi ya Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Esperance ya nchini Tunisia uliyochezwa Mei 24 nchini Morocco , CAF kupitia kamati yake ya waamuzi imetangaza kuamua kumsimamisha kwa miezi sita mwamuzi wa mchezo huo Gehad Grisha .
Mwamuzi huyo kutoka Misri amepewa adhabu hiyo kufuatia kiwango duni alichokionesha katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1 .
.
Mchezo huo ulimalizika kwa Wydad kumaliza wakiwa wachezaji 10 uwanjani kutokana na nahodha wao Brahim Nakach kutolewa kwa kuoneshwa kadi ya pili ya njano uwanjani dakika ya 49, kadi hizo mbili za njano alizipata ndani ya dakika tano.
Mwamuzi huyo alitoa kadi za njano nne katika dakika 45 za kwanza, na katika mchezo huo alienda katika VAR mara mbili, mara ya kwanza alienda na kutoa maamuzi ya kulifuta goli la wenyeji kufuatia mpira kushikwa kabla ya goli kufungwa, na mara nyingine Wydad tena wakanyimwa penati katika dakika ya 57 baada ya kuangalia VAR.
Wydad wakapeleka CAF malalamiko yao juu ya uchezeshaji wa mwamuzi huyo na siku mbili baadae shirikisho hilo la soka limetangaza kumfungia mwamuzi huyo ambaye alichezesha kombe la Dunia 2018.
Mechi ya marudiano ya fainali itapigwa Jumamosi hii Juni 1 nchini Tunisia.