Klopp awashinda City nje ya uwanja
Kupitia haki za matangazo ya Televisheni, timu ya Liverpool imeingiza pesa nyingi zaidi katika Ligi Kuu ya nchini England msimu wa 2018/2019 licha ya kukosa Ubingwa na taji hilo kuchukuliwa na Manchester City kwa mara ya pili mfululizo.
Kati ya vilabu 20 vinavyoshiriki Ligi Kuu ya nchini England,Liverpool ndiyo imekuwa klabu namba moja kwa kuingiza pesa nyingi zaidi kupitia haki za matangazo ya televisheni msimu huu kuliko timu yoyote ile.
Liverpool wameingiza jumla ya pauni milioni 152.5 huku Mabingwa Manchester City wakiingiza pauni milioni 151.
Liverpool sababu ya kuingiza pesa nyingi zaidi ya vilabu vingine 19 vya Ligi Kuu ya nchini humo ni kutokana na wao kuwa klabu maarufu zaidi kwa watangazaji kuliko timu yoyote ile msimu wa 2018/2019, mechi zilizokuwa zinahusisha Liverpool zilikuwa zimeoneshwa mara 29 katika vituo vya Sky Sports na BT Sport , mechi mbili zaidi ya timu yoyote.
Manchester United ambao mechi zao zimeoneshwa mara 27, wameingiza kiasi pauni milioni 10 pungufu na cha Liverpool baada ya kuwa na msimu usio mzuri.