Warriors waendelea kichapo NBA
Ni ushindi wa tisa msimu huu kwa mabingwa watetezi Warriors na wa saba mfululizo.
Katika uwanja wao wa nyumbani Oracle Arena, Golden State Warriors wanaondoka na ushindi wa pointi 116-99 dhidi ya Wolves.
Kwa kawaida Warriors humaliza mechi yao katika robo ya tatu ya mchezo, lakini leo mambo yameenda ndivyo sivyo baada ya Wolves kufufuka kipindi cha pili na kuanza kuusaka ushindi.
Kevin Durant ndiye alionekana kung’aa zaidi kwenye mechi hii akifunga jumla ya Pointi 33, Rebounds 13, huku staa mkubwa wa timu hiyo Stephen Curry akitupia pointi 28 , Rebounds 9, Assist 7 na pointi tatu 4.
Klay Thompson amefunga pointi 22, pia alifunga pointi 3 mfululizo mwanzoni mwa robo ya nne na kuisaidia Warriors kuwa mbele kwa pointi 91-89 ikiwa imebaki dakika 10:17 za kucheza.
Nyota wa Wolves Derrick Rose amecheza dakika tano tu katika robo ya kwanza na kufunga pointi tatu, baada ya hapo hakurejea kwenye mchezo kutokana kusumbuliwa na goti lake la kushoto zikiwa zimepita siku mbili tu tangu MVP huyo wa 2011 afunge pointi 50 katika ushindi dhidi ya Utah Jazz.
Andrew Wiggins ndiye aliyekuwa kinara wa ufungaji katika upande wa Wolves, akifunga pointi 22, huku Jimmy Butler ambaye kocha alimpumzisha siku ya jumatano, ameondoka na Pointi 22.
Katika mechi kumi ambazo Warriors wamecheza msimu huu, wamepoteza moja tu na kushinda tisa. Mpaka sasa Warriors wanaonekana kuzidi kuwa imara na kutokuwa na mpinzani mkubwa katika mbio za kuutetea ubingwa wao.