FA yatengeneza makombe mawili kwa ajili ya City na Majogoo
Bado ngoma nzito nchini England na mchuano ni mkali kweli kweli kati ya Liverpool na Manchester City kujua timu gani itatwaa Ubingwa kutokana na timu hizo kutofautiana alama moja huku michezo wakiwa wamebakiza mitatu kila mmoja.
Chama cha soka England FA kipo katika wakati mgumu wa kujua ni timu ipi itaondoka na taji hilo, linalowindwa na Liverpool ambao hawajalitwaa kwa miaka 29 wakati Manchester City wao wakipambania kutaka kulitetea baada ya mwaka jana kutwaa taji hilo.
Kutokana na sintofahamu FA wanaamini kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa timu hizo bingwa kufahamika katika mechi zao wao za mwisho, hivyo imeandaa makombe mawili katika viwanja viwili na medali ili timu itakayoshinda ipewe taji lake, Man City wanaongoza kwa alama 89 wakifuatiwa na Liverpool wenye alama 88.
Liverpool watakuwa wenyeji wa Wolves siku ya mwisho wakati City watasafiri kwenda kucheza na Brighton. Umbali kati ya viwanja hivyo ni maili 270.
FA imeamua kurudia njia hiyo waliyoitumia mwaka 2012 ambapo City na Man United walikuwa wakiwania ubingwa, wakaenda kucheza mechi zao za mwisho wakiwa tofauti kwa magoli. City akiwa Etihad akicheza na QPR huku United akiwa ugenini kucheza na Sunderland.
Makombe yalitengenezwa mawili na medali, lingine likaenda Etihad lingine Stadium of Light, mwishoni City akaibuka bingwa