Joey Barton amtoa meno kocha mwenzake
Ukiachana na jina la Mario Balotelli ambaye amekuwa na matukio ya ajabu na kuonesha utukutu wake wa hali ya juu kwa makocha na baadhi ya watu wake wa karibu, kuna nyota wa England anayejulikana kwa jina la Joey Barton nae amekuwa na tabia za kitukutu kama ilivyo kwa Balotelli.
Joey Barton ambaye ana umri wa miaka 37 kwa sasa ni kocha wa timu ya Fleetwood Town inayoshiriki Leugue One ya nchini England, hiyo ni baada ya Barton kucheza soka katika vilabu mbalimbali kama Manchester City, Newcastle, QPR, Marseille, Burnley na Rangers.
Jasiri haachi asili . Kiungo huyo wa zamani wa England amerudi kwenye vichwa vya habari tena baada ya kumshambulia kocha wa Barnsley Daniel Stendel na kumsababishia kuhitaji huduma ya dharura ya kumtibu meno baada ya kupigwa kichwa na kuachwa akitema damu huku meno yake mawili yakidaiwa kutoka.
Tukio hilo limedaiwa kutokea kwenye tunnel baada ya mchezo dhidi ya timu wanazozifundisha April 13 ambapo Barton alimfanyia uhuni huo kocha mwenzake, mchezo dhidi yao ulikuwa umemalizika kwa Barnsley ambao walikuwa wenyeji kupata ushindi wa mabao 4-2.