Msuva atoa mtazamo wake kuhusu kundi la Tanzania AFCON 2019
Tanzania imepangwa Kundi C katika kushiriki michezo ya fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika 2019 nchini Misri itakayoshirikisha jumla ya timu 24, Tanzania ipo Kundi moja na Senegal ambao wanajiita Simba wa Teranga, Algeria ambao wanajulikana kama Mbweha wa Jangwani na Kenya Harambee Stars.
Kundi hilo sio jepesi na baadhi ya watu wameanza kuweka utabiri wao kwa kuona timu za Senegal na Algeria ambao wapo juu katika viwango vya soka vya FIFA, zitacheza 16 bora ya michuano hiyo huku wakizipa nafasi ndogo sana Tanzania na Kenya.
Nyota wa Tanzania anayecheza Difaa El Jadid ya nchini Morocco Simon Msuva ameelezea mtazamo wake kuhusiana na Kundi hilo huku akieleza kuwa timu zote zina nafasi licha ya wao kuwaheshimu Senegal, Algeria na Kenya haina maana kwamba wataenda Misri wakiwa dhaifu.
“Kwa upande wangu hili Kundi tulilopangiwa Senegal ni timu nzuri , Algeria ni timu nzuri hata Wakenya pia siwezi kuwadharau ni timu nzuri kikubwa sisi tutajipanga kwa uwezo wetu kama wachezaji najua viongozi nao watajipanga na mashabiki pia sisi ndio watu wa mwisho kuleta matokeo” amesema Simon Msuva