Al Ahly waanza hujuma dhidi ya Mamelodi
Wakati Simba wakiwalalamikia CAF kwa waamuzi wa mchezo wao wa marudiano na TP Mazembe kubadilishwa, timu ya soka ya Mamelod Sundowns ya nchini Afrika Kusini nao wameanza kutoa lawama zao kupitia chama chao cha soka nchini Afrika Kusini kuelekea shirikisho hilo la mpira wa miguu Afrika kuhusiana na mabadiliko ya uwanja wa mchezo wao wa marudiano dhidi ya Al Ahly.
Mchezo wa marudiano wa robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kati ya Mamelodi dhidi ya Al Ahly ulikuwa umepangwa kucheza mjini Suez,Misri lakini kuhamishwa ghafla kwa mchezo huo ikidaiwa kinyume na taratibu kunaleta hofu kwa wapinzani wa Al Ahly ambao ni Mamelodi.
Inadaiwa kuwa Al Ahly baada ya kufungwa kwa mabao 5-0 dhidi ya Mamelodi katika mchezo wa kwanza nchini Afrika Kusini, sasa ameanza kutumia mbinu mbadala za kuhakikisha hang’oki mapema katika michuano hiyo ikiwamo hiyo ya kuhamisha mchezo na kuupeleka katika mji wa Alexandria katika uwanja wa Borg-Al-Arab ambapo ni umbali wa Kilomita 350 kutoka uwanja wa ndege wa Cairo na sio kuchezwa katika mji wa Suez kama ilivyokuwa imepangwa mwanzo.
Sheria za CAF zinaeleza kuwa uwanja wa mchezo unatakiwa kilomita 200 kutoka Airport ambayo timu wageni itashukia, hivyo hii itakuwa ni uvunjaji wa sheria.
Pia sheria za CAF zimekuwa zikieleza kuwa tarehe, uwanja na siku ya mchezo vinatakiwa kutangazwa siku 10 kabla ya mchezo, baada ya hapo hauwezi kubadilisha, kama CAF watakuwa wameruhusu hilo ambapo uamuzi huo umefanywa siku tatu kabla ya mechi itakuwa ni kinyume na sheria na hii inazidi kuchochea moto katika tuhuma dhidi yao kuwa CAF wanapenda kuvipendelea vilabu vya Afrika Kaskazini.