Mbaraka Yusuph nje ya uwanja miezi tisa
Mshambuliaji wa Klabu ya Azam Mbaraka Yusuph atakaa nje ya Uwanja kwa muda wa miezi tisa ijayo baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti jijini Cape Town, Afrika Kusini jana.
Mbaraka amekutwa na tatizo la kuchanika mtulinga wa kati wa goti lake la mguu wa kulia (Anterior Cruciate Ligament Tear), hali iliyolazimika afanyiwe upasuaji huo.
Mchezaji huyo aliyepata majeraha hayo wakati akiwa kwenye kikosi cha Namungo kinachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), iliyomchukua kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu amefanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo nchini humo.
Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, aliyeongozana na mshambuliaji kwaajili ya kushughulikia matibabu yake, ameuambia mtandao rasmi wa klabu hiyo kuwa Yusuph anaweza kurejea tena dimbani kwa ajili ya ushindani mwezi Desemba mwaka huu.