Kocha mwingine wa Sevilla apatwa na kansa
Kocha wa klabu ya Sevilla ya nchini Hispania Joaquin Caparros ametangaza wazi kuwa anasumbuliwa na kansa ya damu ambayo kitaalam inajulikana kama ‘Chronic leukaemia’ .
Mhispania huyo amesema hawezi kustaafu kufundisha soka ataendelea na majukumu yake huku akipambania afya yake.
Joaquin Caparros amesema mpaka sasa hajaanza kupata matibabu yoyote na anachokitaka ni kuendelea kuifurahia kazi yake
Chronic Leukemia ni aina ya kansa ambayo hukua polepole na mara nyingi haitakiwi kutibiwa mara moja unapoipata.
Huu ni msimu wa pili mfululizo kocha mkuu wa Sevilla kupatwa na ugonjwa wa kansa.
Kocha Eduardo Berrizo alipatwa na kansa ya kibofu Novemba 2017 na baadae kufukuzwa mwezi mmoja baada ya kurudi kutoka kufanyiwa upasuaji kutokana na muendelezo wa matokeo mabaha. Kocha huyo sasa ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya Paraguay.
Joaquin na timu yake Sevilla wanashika nafasi ya tano katika ligi kuu nchini Hispania msimu huu wakiwa na pointi 50 huku zikiwa zimebaki mechi saba msimu kumalizika.