Kelele za ubaguzi hazimsumbui Sterling
Ni siku chache zimepita toka nahodha wa timu ya taifa ya England Harry Kane atangaze kuwa atatoa timu uwanjani wakati wa mchezo kama wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya England wenye rangi nyeusi wakiendelea kubaguliwa kama ilivyowatokea dhidi ya Montenegro katika mchezo wa kuwania kufuzu Euro 2020
Baadhi ya wachezaji wa England waliokuwa wamebaguliwa wakati wa mchezo dhidi ya Montenegro uliomalizika kwa England kupata ushindi wa 5-1 ni pamoja na Danny Rose na Raheem Sterling.
Kwa upande wa Raheem Sterling ameweka wazi msimamo wake na kuonekana kuwa amekomaa kisaikolojia na kelele za ubaguzi wa rangi au kubaguliwa hakuwezi kumsumbua hata kidogo zaidi ya kumfanya aongeze nguvu kwani mama yake alishamuandaa.
“Mama yangu alinifundisha namna ya kujipenda mwenyewe na kuipenda rangi ya ngozi yangu na kuwa huru na rangi yangu, mimi ni miongoni mwa watu waliokubaliana na hilo, kutoka nje ya uwanja wakati wa mchezo kama kundi sio kitu sawa, tunatakiwa kushinda mchezo ndio kitu kizuri” alisema Sterling kuelekea mechi ya robo fainali klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Tottenham.