Icardi arejea mzigoni Inter Milan
Mara ya mwisho mshambuliaji Mauro Icardi kuichezea Inter Milan ilikuwa Februari 9 mwaka huu waliposhuka dimbani kucheza na Parma.
Kocha wa Inter Milan Luciano Spalletti sasa amethibitisha kuwa Muargentina huyo amerejea katika kikosi chake na atakuwepo kwenye kikosi kitakachocheza na Genoa kesho Jumatano.
Icardi alivuliwa unahodha wa timu mwezi Februari kufuatia mvutano wa makubaliano ya mkataba mpya, na baadae akadai hatoweza kucheza kwa sababu ana maumivu ya goti.
Baada ya kupoteza unahodha,Icardi hakwenda mazoezini kwa wiki sita zilizofuata.
Wiki jana Icardi karejea mazoezini mara baada ya kikao cha klabu na mwanasheria wake Paolo Nicoletti, na kesho atakuwepo katika mechi ya Serie A ugenini dhidi ya Genoa.
Inter Milan wanashika nafasi ya tatu katika Serie A wakiwa na pointi 53, wakipitwa pointi 10 na Napoli waliopo nafasi ya pili, na pointi 25 nyuma ya Juventus walio nafasi ya kwanza.